Sunday 3rd, November 2024
@Biharamulo
MRADI WA KILIMO BORA CHA MIGOMBA LENYE EKARI MBILI (2)
GHARAMA ZA MRADI
Mradi huu ulianzishwa tarehe 27/12/2017 kwa kupanda migomba ya kisasa aina ya FHIA 17 na FHIA 23 lenye jumla ya miche 888, lengo la kuanzisha kilimo hiki ni kuinua hali ya kiuchumi na familia kwa ujumla. Mpaka sasa mradi huu umeghalimu Tsh. 4,780,000/=. Gharama hizi zinajumuisha maandalizi ya shamba, uchimbaji wa mashimo, ununuzi wa samadi, ununuzi wa miche bora, palizi, ununuzi wa nyasi za kutandazia shamba pamoja na usafi wa shamba kwa ujumla.
HALI YA UZALISHAJI WA MIKUNGU YA NDIZI
Mradi huu kwa sasa una uwezo wa kuzalisha mikungu 800 kwa mwaka, yenye uzito wa wastani wa kilo 50 kwa kila mkungu na zenye wastani wa bei ya kuuzia ya Tsh.8000/= kwa mkungu na matarajio ya kunipatia wastani wa Tsh. 6,400,000/= kwa mwaka.
Mradi huu umekuwa chanzo cha mapato kwa familia, pia umenisaidia kutoa ajira katika jamii, zaidi ya watu 49 (Me 19 na Ke 30) wamepata ajira katika mradi huu tangu maandalizi ya shamba hadi sasa. Kazi zilizofanyika ni pamoja na uchimbaji wa mashimo, palizi, usombaji wa mbolea (samadi) na kupunguzia miche. Aidha, Wakulima 8 wamenufaika na uwepo wa shamba hili kwa kupata zaidi ya miche 1776 na kwenda kupanda kwenye mashamba yao kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha migomba.
Mafanikio ya mradi huu yametokana na ushauri wa Wataalamu wa Ugani katika kata hii ya Nyabusozi. Matarajio yangu ni kuongeza uzalishaji na kufikia mapato ya Tsh. 8,000,000/= kwa mwaka. Hakika kilimo hiki kitanisaidia sana kuboresha maisha yangu.
MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA MAHAKAMA YA MWANZO – STENDI - DDH KM MOJA (1)
Mradi huu umetekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutumia fedha za mfuko wa Barabara, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa ahadi ya Mhe.Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 tulijenga kilometa moja (1) ya Barabara kwa kiwango cha lami ambayo leo tarehe 01/05/2019 tunaomba izinduliwe na Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa.
Mradi huu umetekelezwa na mkandarasi M/S KAJUNA INVESTIMENT COMPANY LTD na ulianza tarehe 02/02/2018 na umekamilika tarehe 28/06/2018, kwa gharama ya Tshs. 298,186,000/= ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la Thamani (VAT.)
HALI YA UTEKELEZAJI.
Hadi sasa mradi huu umekamilika kwa hatua zote zilizoidhinishwa kwenye mkataba ambazo ni ujenzi wa tabaka la kwanza la barabara (Sub grade), tabaka la pili la ujenzi wa barabara (Sub base), ujenzi wa tabaka la tatu la barabara (Base course) pamoja na kuweka lami (Wearing course) pamoja na ujenzi wa mifereji ya mawe (stone pitch) yenye urefu wa 800m2, na mradi huu kwa sasa upo chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi tarehe 28/06/2019.
FAIDA ZA MRADI HUU.
Baadhi ya faida ambazo wananchi watanufaika nazo kutokana na ujenzi wa barabara ya lami ni pamoja na;-
1. Barabara itadumu kwa muda mrefu bila matengenezo ya mara kwa mara
2. Barabara itapitika kwa urahisi wakati wote
3. Barabara imeondoa vumbi kwa watumiaji
4. Barabara ya lami imeboresha usafiri, usafirishaji na mandhari ya Mji.
MRADI WA UKARABATI KITUO CHA AFYA NEMBA
Mradi huu wa ukarabati na Ujenzi wa Kituo cha Afya Nemba ulianza tarehe 01/09/2018 baada ya Halmashauri kupokea fedha kutoka Serikali Kuu kupitia programu ya uboreshaji wa Miundombinu ya kutolea huduma za Afya. Kiasi cha fedha kilichopokelewa ni Tsh.400,000,000/= kwa ajili ya Ukarabati na Ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Nemba.
LENGO LA MRADI
Ni kusaidia wananchi wapatao 20,189 kupata huduma za Afya kwa karibu na kwa urahisi zaidi, Kuondoa au kupunguza vifo vya Mama Wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, Kupunguza vifo visivyo vya lazima pale mgonjwa anaposhindwa kwenda umbali mrefu kufuata huduma za Afya na Kuinua kiwango cha uchumi na uzalishaji kwa wananchi.
VIPENGELE VYA MRADI
Mradi huu unahusisha ujenzi wa majengo yafuatayo:
i. Ujenzi wa Nyumba ya Mganga
ii. Ujenzi wa Maabara
iii. Ujenzi wa Wodi ya Watoto
iv. Ujenzi wa Nyumba ya kuhifadhi maiti
v. Ujenzi wa Wodi ya Wazazi na Jengo la Upasuaji
GHARAMA ZA MRADI
Mradi huu umegharimu kiasi cha Tsh.411,400,000/= ambapo kiasi cha Tshs. 400,000,000/= ni fedha kutoka Serikali Kuu na Tshs. 11,400,000/= ni Mchango wa Jamii katika kusafisha eneo, uchimbaji wa Msingi na ujazaji wa kifusi majengo yote yaliyojengwa.
MRADI WA UBORESHAJI MIUNDOMBINU YA MAJI KATIKA MJI WA BIHARAMULO
Kutokana na umuhimu wa maji kwa viumbe hai ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 unasema “Maji ni Haki ya kila mtu, Tutunze vyanzo vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
Mradi huu wa ujenzi wa miundombinu ya maji ulianza tarehe 26/06/2018 baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA kupata kibali cha kusaini Mkataba wa Tshs 374,508,400 na Kampuni ya Evax Construction LTD ya Wilayani Muleba. Mradi huu wa maji una mtandao wenye urefu wa km 6.58 katika eneo la Ng’ambo.
LENGO KUU LA MRADI
i. Kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa kuweka bomba kubwa lenye kipenyo cha 150mm.
ii. Kufunga bomba la urefu wa km 3.65 kupeleka maji (raising main) kutoka eneo la Kagango hadi eneo la Ng’ambo kwenye tanki la kuhifadhia maji lenye mita za ujazo wa 130.
iii. Kupanua miundombinu ya usambazaji maji kwa kujenga mtandao wa maji wenye mabomba yenye vipenyo tofauti.
iv. Kuongeza vituo viwili (2) vya kutoa huduma ya maji eneo la Ngámbo.
WALENGWA
Walengwa wa mradi huu ni wakazi wote wa eneo la Ng’ambo wapatao 6,511.
GHARAMA ZA MRADI.
Gharama za mradi huu hadi hatua hii umegharimu kiasi cha Tsh. 374,508,400/= kwa mchanganuo ufuatao,
MRADI WA UJENZI WA VYUMBA VIWILI VYA MADARASA NA BWENI KWA AJILI YA WANAFUNZI WA KITENGO CHA ELIMU MAALUM SHULE YA MSINGI KABINDI
Kitengo hiki cha Elimu Maalumu kilianzishwa hapa shuleni mwaka 2014 na kinaendelea kujengeka na kuimarika mwaka hadi mwaka. Hivi sasa kitengo kina wanafunzi 78 ikiwa wavulana 38 na wasichana 40, ambao wapo katika makundi matatu ambayo ni Walemavu wa akili 20 (Wavulana 10 na wasichana 10), Wasiosikia 54 (Wavulana 28 na Wasichana 26), wenye uoni hafifu 2 (Mvulana 1 na Msichana 1) na wenye usonji 2 (Mvulana 1 na Msichana 1).Mradi huu wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na bweni ulianza tarehe 03.09.2018 baada ya Halmashauri kupokea fedha kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
LENGO LA MRADI
Kuboresha mazingira kwa wanafunzi 80 wasichana kulala katika bweni na wanafunzi 50 kusoma katika vyumba viwili vya madarasa. Aidha wanafunzi 28 wataendelea kusoma katika chumba cha darasa kimoja (1) cha zamani.
GHARAMA ZA MRADI
Ndugu, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru,
Halmashauri imepokea Kiasi cha Tshs.Tsh.113,217,300/= kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa mchanganuo ufuatao:-
i.Kiasi cha Tsh. 75,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa bweni moja lenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 80 wa kike.
ii.Kiasi cha Tsh. 38,217,300/= kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.
Mtaa wa Bomani
Sanduku la Barua: S.L.P 70
Telephone: 028 2223403
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@biharamulodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya Biharamulo. Haki zote zimehifadhiwa