Mhe. Albert John Chalamila ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, amefanya ziara na kukagua Miradi ya Maendeleo ili kujiridhisha na hali halisi iliyopo.
Miongoni mwa wataalam alioambatana nao katika ziara hiyo iliyoendelea katika Kata za Biharamulo Mjini, Kabindi, Nyamigogo, Nyakanazi na Nyakahura ni Katibu Tawala Msaidizi(M) upande wa Miundombinu, Afisa Habari na Mawasiliano Serikalini wa Mkoa na Afisa Utumishi na Utawala wa Mkoa.
Wengine alioambatana nao ni pamoja na Kaimu Katibu Tawala (W), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Diwani Kata ya Nyantakara, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Wakuu wa Divisheni na Vitengo wa Halmashauri, Kaimu Afisa Tarafa ya Nyarubungo na Wakuu wa Taasisi za Umma.
Kiongozi huyo amekagua miradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika Kata ya Biharamulo Mjini, mradi wa ujenzi wa vyumba tisa (9) vya madarasa Shule ya Sekondari Runazi iliyopo Kata ya Kabindi, Kijiji cha Kikomakoma.
Miradi mingine iliyotembelewa na Mhe. Chalamila ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Vyumba kumi na saba (17) vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nyakanazi iliyopo Kata ya Lusahunga, Kijiji cha Nyakanazi na Mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari iliyopo Kata ya Nyakahura, Kijiji cha Ngararambe.
Wakati huo huo Mhe. Chalamila ametembelea walengwa (38) walioguswa na Mradi wa Bomba la Mafuta na kuongea na Wananchi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Kasozibakaya Kata ya Nyamigogo.
Chalamila amepongeza wasimamizi wote wa miradi yote aliyotembelea na kuagiza wataalam wa Mkoa watembelee miradi yote hasa yenye madarasa mengi mfano Nyakanazi na Runazi Sekondari zenye madarasa 17 na 9 na kutoa ushauri wa kitaalam inapo bidi kufanya hivyo.
“Mhandisi tembeleeni haraka hizi Shule zenye miradi mikubwa kama hii Shule ya Nyakanazi imepokea Tshs. 340,000,000 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 17 ili mtoe ushauri wa kitaalam pale inapobidi kufanya hivyo ”
Ameyasema hayo leo tarehe 30 Novemba 2022 akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani Biharamulo siku ambayo ameitumia kuwakumbusha wafanyakazi wa Halmashauri kuhudumia wananchi, Walimu wajitahidi kupunguza divisheni 4 na zero na Wanafunzi wasome kwa bidii ili baadaye washike nyadhifa mbalimbali kama Wakuu wa Mikoa, Wilaya na kada mbalimbali. Amewasistiza wanafunzi wasifanya zinaa kwa kuwa ni chanzo cha mimba za utotoni, magonjwa ya zinaa pamoja na ugonjwa wa Ukimwi.
Mtaa wa Bomani
Sanduku la Barua: S.L.P 70
Telephone: 028 2223403
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@biharamulodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya Biharamulo. Haki zote zimehifadhiwa